Katekesi: shauku ya uinjilishaji: bidii ya kitume: ushuhuda wa mtume paulo: wongofu - | vatican news
Katekesi: shauku ya uinjilishaji: bidii ya kitume: ushuhuda wa mtume paulo: wongofu - | vatican news"
Play all audios:
Shuhuda wa Injili ya Kristo: Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa neema yake, Rej. Gal 1:15,
akakutana uso kwa uso na Kristo Yesu Mfufuka wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo, akakukutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka; akatubu na kumwongokea Kristo,
leo hii ni shuhuda na mtangazaji wa Habari Njema ya Wokovu! NA PADRE RICHARD A. MJIGWA, C.PP.S. – VATICAN. Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13.
Hii ndiyo tema inayoongoza Mzunguko Mpya wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 11 Januari 2023. Hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu
Francisko anasema, Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa, jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu
ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ndio mwelekeo na dira ya utume na maisha
ya Kikristo, vinginevyo, Wakristo wanaweza kujikuta wakijitafuta wao wenyewe katika ubinafsi wao. Bila ya kuwa na shauku ya uinjilishaji, imani itadhohofu na hatimaye, kunyauka na utume
ndicho kiini cha maisha ya mwamini. Kumbe, mzunguko mpya wa katekesi ni kutaka kupyaisha shauku ya uinjilishaji kwa kuzama zaidi katika Maandiko Matakatifu sanjari na Mafundisho Tanzu ya
Mama Kanisa ili kuchota amana na utajiri wa ari, mwamko na bidii ya kitume. Katika mzunguko huu wa Katekesi, Baba Mtakatifu anasema, atajitahidi kuweka mbele ya waamini mifano hai na baadhi
ya mashuhuda wa imani, walioamsha shauku ya Habari Njema ya Wokovu, ili wawasaidie waamini kuwasha tena ule moto wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, uweze kuzijaza nyoyo za waamini wote
mapendo. Ni katika muktadha huu, wakristo wanapaswa kujitahidi katika maisha yao ya kila siku kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo unaoganga, kuponya na kuwaokoa watu
kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Shuhuda wa Injili: Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa. (Vatican Media) HABARI NJEMA YA WOKOVU INATANGAZWA NA KUSHUHUDIWA KWA NJIA YA
MATENDO ADILI NA MATAKATIFU NA WALA SI WONGOFU WA SHURUTI KAMA ALIVYOKAZA KUSEMA, HAYATI BABA MTAKATIFU BENEDIKTO XVI. Huu ndio ushuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, lengo na
hatima ya jicho la huruma na upendo kutoka kwa Kristo Yesu, kazi ambayo inaendelezwa kwa sasa na Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na
mashiko! Kristo Yesu Mfufuka aliwatuma wanafunzi wake akisema “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na
kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt 28: 19-30. “Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye
kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi
baraka. Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa
kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya.” 1 Pet 3:8-12. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyoongoza
Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 22 Machi 2023 kuhusu Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume kwa kujikita zaidi katika mchakato wa
uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda!Uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa na wa Ufalme wa Mungu hapa duniani kwa sababu hii ni
asili na utume wa Mama Kanisa tangu awali, kama anavyokazia Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume wa “Evangelii nuntiandi” yaani “Kutangaza Injili” uliochapishwa tarehe 8 Desemba
1975. Ushuhuda wa imani unamwilishwa katika matendo adili na matakatifu (VATICAN MEDIA Divisione Foto) SHUHUDA WA INJILI YA KRISTO: MTAKATIFU PAULO MTUME NA MWALIMU WA MATAIFA ANAKIRI
KWAMBA, MWENYEZI MUNGU NDIYE ALIMTENGA TANGU TUMBONI MWA MAMA YAKE, AKAMWITA KWA NEEMA YAKE, Rej. Gal 1:15, akakutana uso kwa uso na Kristo Yesu Mfufuka wakati akiwa njiani kuelekea Dameski,
akienda kuwadhulumu Wakristo. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea kwa kina wito wa Sauli, jinsi alivyoitwa na Kristo Yesu, akamwongokea Mwenyezi Mungu, toka katika upofu wa mwili,
akabahatika kuuona Mwanga wa kweli, Kristo Yesu Mfufuka, akawa kweli ni chombo kiteule cha Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Jina la Mungu kwa watu wa Mataifa. Rej. Mdo 9:15. Katekesi ya
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 29 Machi 2023 imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu inayoonesha kiri ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayethibitisha kuhusu
wito wake akisema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile
aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Huu ndio ushuhuda wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, akionesha shauku ya uinjilishaji na bidii ya kitume,
baada ya kutubu na kumwongokea Kristo Yesu. Kutoka katika Torati akaikumbatia Injili; Yeye ambaye ambapo mwanzo alitaka kulidhulumu na kulibomoa Kanisa, sasa anakuwa ni shuhuda wa ujenzi wa
Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa, kiasi kwamba, sasa anataka kujisadaka kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Paulo Mtume alikirimiwa zawadi ya toba na wongofu wa ndani
(Vatican Media) PAULO KWA KUKUTANA NA KRISTO MFUFUKA AKAMKIRIMIA ZAWADI YA TOBA, WONGOFU WA NDANI NA UPENDO THABITI KIASI HATA CHA KUJISADAKA BILA YA KUJIBAKIZA KUMTANGAZA NA KUMSHUHUDIA
KRISTO YESU kwa watu wa Mataifa. Paulo Mtume, kwa kukutana na Kristo Mfufuka, maisha na wito wake ukachukua dira na mwelekeo mpya, kiasi cha kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika
mwanga wa Kristo Mfufuka. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hivi ndivyo inavyotokea wakati wa mageuzo ya mkate na divai, kuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo
Yesu, lakini mkate na divai inaendelea kubaki katika maumbo yake asilia. Mababa wa Kanisa wanasema, kwa mageuzo ya mkate na divai hufanyika mabadiliko ya uwamo wote wa mkate katika uwamo wa
Mwili wa Kristo, Bwana wetu, na uwamo wote wa divai katika uwamo wa Damu yake. Kanisa Katoliki kwa haki na usawa limeyaita mabadiliko haya “mageuzo-uwamo” (transsub-stantiatio). Rej. KKK
1373-1377. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anauhitaji hata ubinadamu wako, jambo la msingi ni ule wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuwa ndani ya Kristo Yesu na hivyo kuwa ni kiumbe: ya kale
yamepita: tazama! Yamekuwa mapya! Re. 2Kor 5:17. Baba Mtakatifu anaonya kwamba, haitoshi kusoma na kufaulu katika Taalimungu au Sayansi ya Maandiko Matakatifu, kama mwamini hana wongofu wa
ndani ni kazi bure! Ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu! Waamini wakitaka kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu, wajenge utamaduni wa kusali, kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la
Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wasimike maisha yao katika ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Mchakato huu, uwawezeshe waamini kuuvua utu wa kale na
kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka kiasi cha kuwashangaza jirani zao, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, sasa ni kielelezo na ushuhuda wa huruma
na upendo wa Kristo Yesu unaoganga na kuokoa. Upendo wa Kristo unaponya na kuokoa! (Vatican Media) BABA MTAKATIFU ANAKAZA KUSEMA KATIKA ULIMWENGU MAMBOLEO KUNA HAJA YA KANISA KUWA NA
MASHUHUDA WANAOTHUBUTU KUENDELEA KUSALI NA KUSAMAHE, KAMA MFANO BORA WA KUIGWA. Kati ya watu walioombewa na Stefano alikuwepo pia kijana Sauli aliyeona na kushuhudia vyema kuuawa kwake.
Lakini baadaye kwa njia ya neema ya Mungu, Sauli akatubu na kumwongokea Mungu, akageuka kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa; mmisionari aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na
kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Paulo amezaliwa upya kwa neema ya Mungu na kwa njia ya ushuhuda wa msamaha wa Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi,
kiasi kwamba, amekuwa ni mbegu ya toba na wongofu wake. Huu ni ushuhuda kwamba, matendo ya huruma na mapendo, ni cheche zinazoweza kuleta mageuzi makubwa katika historia ya maisha ya
mwanadamu. Mtume Paulo anashuhudia akisema yote haya ni sifa kwa rehema kutoka kwa Kristo Yesu: “Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu,
akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani.
Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni
awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale
watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele. Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.” 1Tm
1:12-17. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi yake, kwa kuwataka Wakristo kukita maisha yao katika toba na wongofu wa ndani, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa huruma na
upendo wa Kristo Yesu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Paulo Mtume
Trending News
Papa:wayahudi na wakristo wanaokiri muumba mmoja wanaweza kufungua njia za amani! - | vatican newsKatika mkutano na wawakilishi wa Jukwaa la Kimataifa la Kiyahudi,Papa Francisko amebainisha kwamba kila vita siku zote,k...
404 - ukurasa haujapatikanaNenda kwenye maudhuiNenda kwenye orodha kuuNenda tovuti zaidi za DWVidio zetuSauti zetuMaeneoTanzaniaKenyaJamhuri ya Kid...
Katekesi: shauku ya uinjilishaji: bidii ya kitume: ushuhuda wa mtume paulo: wongofu - | vatican newsShuhuda wa Injili ya Kristo: Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimtenga ...
Latests News
Katekesi: shauku ya uinjilishaji: bidii ya kitume: ushuhuda wa mtume paulo: wongofu - | vatican newsShuhuda wa Injili ya Kristo: Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimtenga ...
404 - ukurasa haujapatikanaNenda kwenye maudhuiNenda kwenye orodha kuuNenda tovuti zaidi za DWVidio zetuSauti zetuMaeneoTanzaniaKenyaJamhuri ya Kid...
Papa:wayahudi na wakristo wanaokiri muumba mmoja wanaweza kufungua njia za amani! - | vatican newsKatika mkutano na wawakilishi wa Jukwaa la Kimataifa la Kiyahudi,Papa Francisko amebainisha kwamba kila vita siku zote,k...